TUJADILI KUHUSU SULUHISHO LA UBORESHAJI WA SEKTA YA TAKA NGUMU TANZANIA.
UTANGULIZI
Maboresho ya usimamizi wa Sekta ya taka ngumu ni fursa kubwa kwa watanzania katika jitihada za kuendana na mageuzi mapya ya kukuza uhusiano wa kuishi kulingana na malengo endelevu ya dunia katika kuchochea mazingira himilivu na endelevu yanayoweza kikamilifu na kwa ufanisi kukabiliana na athari za uchafuzi wa mazingira na janga la mabadiliko ya tabianchi ( Climate change).
Sera ya mazingira ya taifa ya mwaka 2021 imehusianisha moja kwa Moja Utawala Bora na Usimamizi wa mazingira. Katika sura ya kwanza, kipengele cha pili, kifungu Cha tisa inasema kwamba, Utawala Bora ni nguzo muhimu Kabisa “central component” katika Usimamizi wa mazingira. Pia miongoni mwa malengo ya Sera hii ni kuhamasisha utawala Bora kwenye Usimamizi wa mazingira katika ngazi zote za uongozi. Utekelezaji wa sera hii umechochea ushirikishwaji wa wananchi katika mipango ya Usimamizi mazingira, na pia kuajiriwa kwa maafisa mazingira katika ngazi ya wizara, mikoa,wilaya mpaka ngazi ya kata.
Sera hii pia imehimiza ushirikishwaji wa sekta binafsi, wadau wa maendeleo, mashirika ya Kidini na asasi za kiraia katika kusaidia Usimamizi wa mazingira. Mashirika mengi yamejikita katika kuratibu Usimamizi wa taka ngumu hasa za plastiki na takaozo. Makundi mbalimbali ya vijana na kina mama pia yamejiingiza katika biashara ya ukusanyaji na usafirishaji wa taka ngumu kutoka katika maeneo yanapozalishwa na kupelekwa Dampo.
Sehemu ya pili ya Sheria ya mazingira ya mwaka 2004 inataka katika kila ngazi ya utawala kuwepo na afisa mazingira(na vigezo anavyopaswa kuwa navyo) ambaye majukumu yake pamoja na kamati ya Mipango miji ni kuhakikisha Sheria hii inatekelezwa kikamilifu.
USIMAMIZI WA TAKA NCHINI
Taarifa kutoka ofisi a takwimu taifa (NBS 2017b) zinathibitisha ni tani 4,700 huzalishwa kwa kila na kadili nchi inavyozidi kuwa kwenye viwango vya juu kiuchumi, makadilio yanatoa utabiri wa kuongezeka kwa uzalishaji wa taka kufikia mpaka tani 12,000 kufikia 2025.
Aidha mpango mkakati wa mazingira kitaifa (NEMPSI) National Environmental Master Plan for Strategic Interventions 2022–2032. ambao umeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa lengo la kutoa mwongozo wa kimkakati na uratibu wa shughuli za utunzaji mazingira katika kila ngazi kwa kuzingatia mgawanyiko wa athari za kimazingira na suluhisho. (NEMPSI) imeandika usimamizi wa taka ngumu ni miongoni mwa tatizo kubwa la kimazingira na kwa umma linalokabili majiji na miji ya nchi hii, kutokana kukua kwa miji, uchumi kuimarika na kupelekea kubadili mfumo wa maisha na ulaji, hivyo kusabisha ongezeko kubwa la kiasi cha uzalishaji wa taka. Takwimu za (NEMPSI) kuhusu taka ngumu nchini, karibia tani milioni 7 za taka ngumu huzalishwa nchini kila mwaka, na uzalishaji mkubwa unapatikana kwenye mamlaka za mijini kulinganisha na halmashauri za wilaya nchini.
Jiji la Dar es salaam pekee inakadiliwa kuwa asilimia 40 mpaka 60 ya taka zinazozalishwa hazikusanywi, ukizingatia uzalishaji wa siku moja ni tani 4200 mpaka 4700 kutokana na tafiti mbalimbali, hii inadhihirisha kuna uwiano wa asilimia 50 ya taka ambazo hazizolewi ambazo ni sawa na tani 800,000, na hivyo taka hizo kuchomwa moto, kuzikwa na kutupwa kiholela sehemu mbalimbali za wazi na mifereji ya maji. Kwa uhalisia huu wa ukuaji wa jiji hasa Dar es salaam hadi kufikia 2030 litakuwa ni jiji kubwa, hivyo lazima kuwe na mkakati madhubuti wa uboreshaji wa sekta ya taka ngumu nchini ili kukidhi mahitaji haya.
Kutokana na changamoto kubwa ya taka nchini, taasisi za kiserikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kwa ujumla zimekuwa zikipaza sauti ilikuwa na nguvu ya pamoja katika kukabiliana na kutatua changamoto katika sekta ya taka ngumu nchini ili kukuza uchumi kupitia fursa za zitokanazo na taka ngumu na kufikia lengo kuu la kuwa na mazingira safi salama na yenye afya kwa ustawi wa nchi yetu.
Kuwepo kwa jitihada hizi lakini bado hali ya usafi nchini Tanzania kuhusu udhibiti taka ngumu ni tatizo la muda mrefu ambalo lina changamoto nyingi. Tabia iliyozoeleka miongoni mwa jamii ya utupaji ovyo wa taka katika maeneo yasiyostahili imechangia maeneo mengi kuwa machafu. Kuzagaa kwa taka kunaweza kuwa kichocheo cha milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara na kutapika. Hali ya uchafu nchini inachangiwa pia na elimu ndogo juu ya usafi wa mazingira, kutotii sheria zilizopo kwa upande wa wananchi na usimamizi hafifu wa sheria za usafi wa mazingira.
Katika kudhibiti taka ngumu Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake imetoa mamlaka katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini kusimamia Sheria hiyo. Pamoja na Sheria hiyo kuwa wazi na kutoa mamlaka katika Halmashauri na Serikali za Mitaa kuhusu udhibiti wa taka ngumu, lakini bado kuna changamoto nyingi katika usimamizi. Zifuatazo ni changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya taka ngumu;
CHANGAMOTO NA SULUHISHO LA SEKTA YA TAKA NGUMU TANZANIA
- Miundombinu hafifu ya huduma ya kuzoa na kutupa taka kwenye makazi, vituo vya kukusanya taka na madampo — hali hii inaiweka jamii kwenye hatari hata kama usimamizi wa taka ngumu upo kisheria, pungufu ya asilimia 40 ya kaya hazina huduma ya uzoaji wa taka (Huisman et al., 2016). na kwenye miji zaidi ya asilimia 80–90 ya taka hazikusanywi (NBS, 2017b). Mfano kwa Dar es salaam dampo la pugu limekuwa halingiliki kirahisi hasa nyakati za mvua na kusababisha magari ya taka kukwama kwa muda mrefu. Na mara nyingi wakati wa kukwamua magari hayo hutokea uharibifu mkubwa kwani husukumwa kwa kutumia mitambo ya dampo. Magari yetu yanaharibika kila mara na kupelekea hasara na gharama kubwa za ziada kwa wakandarasi wa kuzoa taka.
SULUHISHO
Kutokana na changamoto kubwa ya maeneo ya kutupia taka katika madampo, ushauri ni kuwepo na mpango endelevu wa kuhudumia madampo haya kwa kutengeneza barabara za kuingia na kutokea dampo na kazi hii iwe endelevu; aidha mitambo ya kuhudumia dampo ipatiwe maboresho na mafuta ya kutosha ili kuwezesha magari yetu kuingia na kutoka bila kikwazo chochote kile kwa nyakati zote.
Kuwekeza katika teknolojia ya kisasa kwa kununua vifaa bora na vya kisasa vya kukusanya taka na pia kutafuta ushirika wa sekta ya umma na binafsi ili kuwezesha upatikanaji wa fedha zinazokidhi kuendeleza na kujenga miundombinu ya kusimamia taka ngumu hasa uboreshaji wa madampo. Jitihada nyingi zinachukuliwa na serikali na wadau wa maendeleo katika kutafuta suluhu la kudumu la tatizo hili, mwaka 2017 kwenye tafiti iliyofanywa na wataalamu wahandisi kutoka uholanzi walitoa mapendekezo yao ya mwongozo wa usimamizi wa taka ngumu nchini na maboresho ya dampo la pugu, katika mwongozo huo unaoitwa Netherlands — Tanzania cooperation on Waste Management (roadmap for waste management in Tanzania), kuna mapendekezo yafuatayo;
- Kuongeza wigo wa huduma ya ukusanyaji taka katika jiji Dar es salaam kufikia kiwango cha chini cha asilimia 90
- Kuongeza ubora na ufanisi wa kukusanya na kusafirisha taka ngumu kwa kutumia vituo vya kukusanyia taka (waste transfer stations)
- Kutibu, kuboresha na kuongeza ukubwa wa dampo la pugu katika viwango vinavyokubalika kwenye madampo ya kisasa na kuongeza muda wa matumizi ya dampo kwa miaka 20 ijayo.
- Kuanzisha mfumo wa kisasa wa kukusanya ada ya taka kwa umma katika namna ambayo itafidia gharama zao za kulipia taka
- Mwisho ni kuanzisha taasisi itakayohusika na usimamizi wa taka Dar es salaam na nchi nzima mfano (establishment of a Metropolitan Waste Authority).
2. Ukosefu wa elimu ya kutunza mazingira kwa umma, mfano kwa mazingira ya sasa bado kunahiajika sana elimu ya umuhimu wa ulipaji wa ada ya taka kwa wananchi, kutenganisha taka na urejelezaji ili kuboresha sekta ya taka nchini.
SULUHISHO
- Mfano vyombo vya habari, wanayo nguvu sana kwenye jamii. Kama maamuzi yakifanyika kwenye hili na wadau wakitoa ushirikaino basi swala la uchafuzi wa mazingira linaweza kuisha kabisa. Mfano, kwenye kila chombo cha habari ukawekwa utaratibu dakika 10 tu za kutoa elimu juu ya kuondokana na uchafuzi wa taka, ikanaoneshwa athari zake, ikatolewa mifano nchi safi na chafu, kwa ufupi kutumia ubunifu wetu na watangazaji wetu kuhakikisha ujumbe unafika.
- Kuwepo kwa programu endelevu za elimu ya utunzaji mazingira na umuhimu wa usimamizi bora wa taka kwenye shule na jamii kwa ujumla itakayotekelzwa nchi nzima. hili litawezekana kwa mamlaka za serikali, taasisi binafsi, mashirika yasiyokuwa ya serikali na wadau wengine wa elimu kufanya kazi kwa ushrikiano ili kupata matokeo bora katika kuboresha sekta ya taka ngumu nchini
- Pia uwepo wa vipindi kwa ajili ya kuonesha ubunifu mbalimbali unaosaidia kuepukana na uchafuzi wa mazingira hiyo itaamsha pia wataalam kuja na mbinu za kuhifadhi uchafu, kuchakata tena uchafu (recycling) au za kuzalisha taka ambazo ni rafiki katika mazingira.
- Kama ambavyo sanaa, mpira wa miguu, masumbwi n.k. vilivyopewa kipaumbele, hili la uchafuzi wa mazingira pia linawezekana kwani nguvu zenu tushaziona zinavoweza kuleta matokeo makubwa kwa jamii.
- Kuongeza ubunifu katika katika sekta binafsi kwa kuhakikisha uzalishaji wao unapunguza uchafu pia kuwe na sera na mikakati ya kwamba moja kati ya harakati za kurudisha kwa jamii “CSR” ihusishe kutatua tatizo la uchafuzi wa mazingira. Mfano, kampuni ikaweka mkakati wa kuhakikisha maeneo yote ya umma yanawekea ndoo za kuhifadhia taka, ziwe za kuweka taka za aina tofauti tofauti kwa ajili ya urahisi wa kwenda kuzichakata tena. Mfano baadhi ya nchi za wenzetu wamewekewa sehemu maalumu ya kuweka chupa za plastik, na unapoweka kila chupa moja ina thamani hivo unaodoka na pesa yako kila unapoweka taka za plastik japo ni pesa ndogo lakini ni motisha!
- Pia jamii na viongozi wa ngazi za chini wajengewe uwezo katika kutambua na kuratibu shughuli zinazoweza kupunguza mzigo wa taka ngumu, maji taka na uharibifu mwingine unaotajwa na sera yetu ya mazingira.
3. Utekelezaji hafifu wa sheria za kukataza utupaji taka ovyo; Kutokana na uhaba wa usimamizi wa sheria kuanzia ngazi ya mtaa mpaka serikali kuu katika kuzuia utupaji wa taka ovyo, umepelekea kuongezeka kwa taka mtaani.
SULUHISHO
- Kuweka kipaumbele katika utekelezaji wa sheria na sheria ndogondogo zinatoa katazo la utupaji taka ovyo mtaani na pia kuwe na kikosi kazi kutoka kwenye mitaa ambacho kitasaidia utekelezaji katika kusimamia sheria.
- Serikali yaani seriakali za mtaa, mamlaka za kiserikali, taasisi za serikali, vyombo vya dola , serikali kuu na wote ambao wako ndani ya kundi la serikali. Tukianza na kuwasimamia mtu mmoja mmoja, serikali ya mtaa inaweza kufanya kazi katika maeneo tunayoishi. Taka zisitupwe ovyo na zikusanywe kwa mpangilio maalumu (yani taka zitenganishwe za chakula kivyake, karatasi kivyake na plastics kivyake n.k.).
- Pia maeneo ya umma, serikali inaweza kushirikisha vyombo vya usalama kusimamia na kuhakikisha wanaokiuka wanafikishwa vyombo vya sheria kwa hatua stahiki. Kama ambavyo imewezekana kuondoa vibanda sehemu zisizoruhsiwa, tumeona mgambo wakifanya kazi yao. Hivo tunaweza kuwatumia pia katika usafi au tukatumia shirikishi.
4. Mfumo hafifu ukusanyaji wa ada za taka na zikikusanywa kuwekwa kwenye akaunti ya halmashauri za manispaa na wakandarasi wanapaswa kuandika barua kuziomba upya, jambo ambalo linapelekea manispaa na halmashauri kukaa na fedha hizo muda mrefu aidha kutokana mifumo ya malipo ya serikali kuwa taratibu na kushindwa kuwalipa kwa wakati wakandarasi na kuzorotesha ufanisi bora katika usimamizi wa sekta ya taka.
5. Uwepo wa jitihada chache katika kupunguza uzalishaji wa taka ngumu nchini; Mamlaka za serikali za mitaa nyingi nchini zinakosa kuwepo kwa mifumo sahihi ya kupunguza taka, kutumia tena na urejelezaji, kitu ambacho kinapelekea kuongezeka kwa gharama za usimamizi wa taka kwa kuzisafirisha kupeleka dampo. Mfano Dar es salaam, ni manispaa ya Kinondoni imeanzisha mitambo ya kutengeneza mboji ili kupunguza kiwango cha taka ozo zinazopelekwa dampo.
SULUHISHO
Ili kupunguza uchafuzi wa mazingira, iandaliwe na iboreshwe sera ya urejelezaji wa taka ngumu ambayo itakuwa ni msingi muhimu kwa Taasisi za Serikali kuanza kutambua na kurasimisha sekta ya urejelezaji taka ambayo awali ilikuwa ikiendeshwa na Taasisi binafsi na vikundi visivyokuwa rasmi. Katika kuhakikisha hilo linafanyika halmashauri na manispaa mbalimbali hapa nchini zifanye yafuatayo;
- Kubuni miradi mbalimbali ndani ya Jiji itakayohusisha wadau mbalimbali inayolenga urejelezaji taka pamoja na masoko ya uhakika ya taka zilizorejelezwa au bidhaa zilizotokana na taka rejea.
- Kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kurejeleza taka ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Halmashauri za Manispaa katika kuhakikisha utenganishaji wa taka unafanyika kuanzia ngazi za uzalishaji (sorting at source).
- Kuwatambua na kuwaunganisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na teknolojia za urejelezaji taka ndani ya Jiji la Dar es Salaam
- Kutenga maeneo ya Viwanda vidogovidogo au karakana (recycling facility) ndani ya dampo au katika maeneo yake ambayo yatafaa kwa kazi zinazohusiana na urejelezaji taka.
- Kuhamasisha teknolojia zinazolenga uzalishaji na utumiaji wa bidhaa zitokanazo na taka rejea.
6. Kuhakikisha inaweka mazingira bora yatakayowezesha ukuaji wa sekta ya urejelezaji taka ngumu kwa kuongeza viwanda na ubora wa bidhaa zake ili ziweze kupata soko ndani na nje ya nchi na hatimaye kukuza pato jamii na Taifa.
7. Kuwezesha wananchi wa maisha ya chini wakiwemo vijana na wanawake kushiriki katika ubunifu na utumiaji wa teknolojia za urejelezaji taka na hatimaye kuweza kuboresha usafi.
FAIDA ZA MFUMO BORA WA USIMAMIZI WA TAKA NGUMU KATIKA MIJI NA MAJIJI MBALIMBALI HAPA NCHINI.
- Kuongeza ushindani unaopelekea ufanisi; endapo sekta binafsi zitapewa vibali bila shida katika kusimamia na kudhibiti taka ngumu katika miji na majiji hapa nchini, kutakuwa na usimamizi imara na kufanya kazi kwa kujituma, taka ngumu zitakusanywa kwa wakati na kwa ushindani ili kuongeza mapato katika taasisi husika. Hivyo changamoto ya kuwa na taka ngumu zinazotelekezwa mtaani litakua limepata suluhu.
- Kuongeza ubunifu na ajira binafsi; endapo kutakua na taasisi nyingi zinazojishughulisha na ukusanyaji wa taka ngumu, ubunifu utaongezeka katika zoezi la ukusanyaji taka ili kuvutia wateja wenye taka hizi. Pia sekta hizi zitaajiri vijana wasio na ajira, hivyo itasaidia kupunguza tatizo la ajira katika nchi yetu.
- Serikali kuongeza mapato yanayotoka na kodi; hii ni kutokana na taasisi binafsi zitakazopewa kibali cha kuthibiti taka zitahusika katika ulipaji wa kodi hivyo serikali kujipatia mapato yatakayosaidia kutatua changamoto mbalimbali katika zoezi la usimamizi taka ngumu pia mapato ya kodi hizi yatatumika katika ujenzi wa nchi yetu.
- Kupungua kwa uharibifu wa miundombinu ya barabara na mitaro; imeshuhudiwa katika miji na majiji mengi yanatokea mafuriko kutokana na mitaro ambayo inahusika kupitisha maji machafu na ya mvua kuziba sababu ya taka ngumu ambazo zinatupwa katika mitaro hiyo, mfano TARURA wanatumia gharama nyingi kila mwaka kuzibua madaraja na mitaro ambayo inaziba sababu ya taka ngumu, fedha hiyo ingetumika kujenga barabara na mitaro mipya katika miji na majiji hapa nchini. Hivyo kama pendekezo hili litanyiwa kazi, miundombinu itakuwa salama na kupunguza gharama za marekebisho kila mwaka ambazo zingetumika kujenga miundombinu mpya.
- Kupungua kwa maambukizi ya magojwa yanayosababishwa na mrundikano wa uchafu; magojwa kama kipindupindu na homa ya matumbo imekua changamoto katika sehemu nyingi Tanzania sababu ya usimamizi mbovu wa taka ngumu, imeshuhudiwa milipuko ya magojwa haya kama Dar es Salaam, Iringa na sehemu nyingine za nchi sababu kubwa ikiwa ni uchafu uliopindukia katika mitaa mbalimbali kutokana na taka zilizotelekezwa. Magojwa haya yamesababisha vifo kwa raia na kuathiri nguvu ya taifa katika uzalishaji. Hivyo ili kupambana na tatizo la mlipuko wa magojwa haya ni vema mamlaka husika kuzingatia mapendekezo haya.
HITIMISHO .
Elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kutunza mazingira, athari za uchafuzi wa mazingira kiafya, kimazingira, kijamii na kiuchumi na elimu hii itolewe kwa ushirikishwaji mkubwa wa jamii hasa wale waathirika wakubwa wa uharibifu wa mazingira na elimu inayotolewa iakisi uhalisia wa mazingira yao, hii ni chachu kubwa katika kuongeza ushiriki na uwajibikaji wa jamii katika utunzaji wa mazingira yao.
Uhamasishaji wa mazoezi kufanya usafi kwenye fukwe, mito, sehemu za wazi, mabondeni na kwenye mifereji. Zoezi la usafi wa kijamii kwenye maeneo tajwa ni muhimu kwa kuwa ndio njia pekee ya kuondoa taka zilizojaa kwenye maeneo haya, huku jitihada za kutoa elimu zikiendelea ili kupunguza kasi kama sio kuzuia kabisa kuendelea kutupwa taka kwenye maeneo yetu. Kufanya usafi wa kijamii ni ishara ya uwajibikaji na uraia mwema katika kutoa mchango katika maendeleo ya ustawi wa jamii zetu. Pia usafi wa kijamii ni hamasa na sehemu ya kukusanya takwimu na taarifa za hali ya uchafuzi ili kutafuta utatuzi wa kudumu wa uchafuzi wa mazingira kwa kuwatambua wachafuzi wakubwa na kutafuta namna bora ya kuwashirikisha katika kuondoa changamoto hii, pia taarifa hizi ni muhimu kwa serikali katika kufanya maamuzi kwenye namna bora ya kuhakikisha tatizo la uchafuzi wa mazingira linakwisha kabisa.
Uwepo wa miundombinu imara katika kudhibiti suala la uchafuzi wa mazingira kama uwepo wa huduma bora ya uzoaji wa taka, kuweka mazingira wezeshi ya uchambuzi wa taka kuanzia kwenye kaya, ili kurahisisha zoezi la urejelezaji wa taka, uwepo wa madampo ya kisasa ya kutupa taka, viwanda vya urejelezaji wa taka ili kuhakikisha taka zote rejelezi haziendi dampo na viwanda vya utengezaji wa mboji inayotokana na takaozo za mabaki ya vyakula na mazao.Hii itapunguza kiasi kikubwa cha taka zinazoenda dampo, ambazo zinamchango mkubwa katika uzalishaji wa hewa ya ukaa (METHANE) ambayo inachangia uharibifu wa utando wa ozone na kusababisha kuongezeka kwa joto duniani na kuleta mabadiliko ya tabia nchi ( climate change).
Ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika kutatua changamoto ya uchafuzi wa mazingira, suala la uchafuzi wa mazingira na athari zake zipo katika kila sekta kuanzia kwenye mazingira, uchumi, miundombinu, elimu, afya, teknolojia nk. Hivyo kutafuta suluhu yake pia lazima sekta zote zihusike kikamilifu, pindi sekta moja inaposhindwa kushiriki hatuwezi kutatua changamoto hii, hivyo kwa serikali yenye mamlaka ya kufanya hili la kuunganisha sekta hizi, iweze kuendelea kuboresha mazingira katika ushirikishwaji mkubwa wa sekta zote linapokuja suala la maamuzi yanayohusu mustakabali wa utunzaji wa mazingira ili tuweze kupata matokeo chanya.
Mwisho napenda kutoa rai kwa wadau wa mazingira, serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuona suala la madhara ya uchafuzi wa mazingira ndio chanzo kikubwa cha mlipuko wa magonjwa mengi kwenye jamii zetu na lazima tuone kuna uhusiano mkubwa sana baina ya afya bora na usafi wa mazingira yetu, kama ikitokea vinginevyo ndio maana tunaona watu wetu wanapata adhabu ya magonjwa, mafuriko na uharibifu mkubwa wa mali zao. Hivyo kwa uongozi wetu tuwasaidie watu wetu kwa kuwapa taarifa za kutosha na sahihi juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kama ndio kichocheo kikubwa katika kujenga jamii yenye afya, safi na salama na hilo ndilo liwe neno katika kuziba mwanya wa ufinyu wa taarifa na takwimu uliopo kwenye vyanzo na kiwango cha athari za uchafuzi wa mazingira katika nchi yetu ya Tanzania.